MENEJA WA JATU MBINGU, AREJEA NCHINI NA KUSIMULIA KWA KINA YALIYOJIRI NCHINI UFILIPINO

 

Na: Mwandishi Wetu

Meneja wa Kampuni ya Jatu Tawi la Mbingu mkoani Morogoro ambalo linajishughulisha na usimamizi wa kiwanda cha kukoboa mchele, Ndugu Paul Kapalata hatimaye amerejea nyumbani Tanzania akitokea nchini Ufilipino na kueleza bayana kuhusu ujuzi alioupata nchini humo.

Meneja huyo ambaye alikuwa nchini Ufilipino tangu June 25, 2018, kwa lengo la kupata mafunzo ya kilimo cha zao la mpunga ambayo yalidhaminiwa na Shirika la Chakula Duniani FAO, na kufanyika katika taasisi ya kimataifa ya utafiti wa mchele iitwayo ‘International Rice Research Institute (IRRI) amesema kuwa, mafunzo hayo yalihusu vipengele vyote vya uzalishaji wa mchele kuanzia maandalizi ya ardhi yaani shambani hadi hatua ya usindikaji baada ya kuvuna.

Aidha, Kapalata ameongeza kuwa malengo makuu ya mafunzo hayo yalikuwa ni pamoja na kujifunza mbinu za uzalishaji wa mchele kisasa, kujua kanuni za uzalishaji endelevu wa mchele pamoja na kupata uzoefu wa hatua zote za ukuaji wa zao la mpunga.

Malengo mengine ni pamoja na kutambua namna ya uzalishaji bora wa mbegu za mchele pamoja na njia za usambazaji wake na kujenga mahusiano na wafanyabiashara wa sekta za kilimo wa Asia. Pamoja na hayo, Kapalata amesema kuwa, mafunzo hayo yalichukua takribani siku 10 darasani na kutawaliwa na majadiliano, mafunzo ya vitendo pamoja na kutembelea ushirika wa wakulima na mabenki wa vyama vya ushirika ambao huunga mkono wakulima kupitia utoaji wa mikopo.

Hata hivyo, Kapalata amesema kuwa , kupitia mafunzo hayo amejifunza mengi kuhusu kilimo cha mpunga hususani yale ambayo awali alikuwa hayafahamu au kuyafahamu kwa kiasi , hivyo baada ya mafunzo haya kukamilika anaamini kwamba elimu aliyoipata italeta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo cha mpunga ndani ya Kampuni ya Jatu na Tanzania kwa ujumla.

Mbali na hayo, Kapalata amewataka wanachama wa Jatu ambao bado hawajajiunga na miradi ya kilimo inayoendeshwa na kusimamiwa na kampuni hiyo, kufanya hivyo sasa kwani mafunzo aliyoyapata nchini Ufilipino ataanza kuyahamishia katika vitendo kupitia miradi ya kilimo hususani kilimo cha mpunga na hivyo kufanya kilimo hicho kuwa na tija na manufaa kwa wanachama wa Jatu pamoja na watanzania wote kwa ujumla. Pia Kapalata ametoa shukrani zake za pekee kwa uongozi wa Jatu Plc kwa kumchagua kuiwakirisha kampuni katika mafunzo hayo, lakini pia Shirika la Chakula Duniani (FAO) pamoja na Serikali ya Tanzania kwa kutoa ruhusa ya kuhudhuria mafunzo hayo.

Shukrani nyingine ametoa kwa Taasisi ya IRRI kwa kuendesha mafunzo hayo kwa kipindi cha wiki mbili, lakini pia kwa namna ya pekee ametoa shukrani kwa Mheshimiwa Kalisa, Dennis Lzaro Londo, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kilombero Halmashauri ya Morogoro), Afisa wa Umwagiliaji wa Kilimo wa Wilaya ya Mohamed Ramadhani na Afisa wa Ushirika ambao walifanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha tunahudhuria mafunzo hayo.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You may use these HTML tags and attributes: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <strike> <strong>