MKUU WA WILAYA YA TEMEKE ABARIKI SAFARI YA JATU KUELEKEA D.S.E

Na: Mwandishi Wetu

Mkuu wa Wilaya ya Temeke ndugu, Felix Lyaniva amesema kuwa, kitendo cha kampuni ya Jatu Plc kuamua kuelekea kwenye Soko la Hisa D.S.E ni jambo nzuri na analiunga mkono na anaamini litachangia kuondoa umasikini kwa jamii na kukuza uchumi kwa ujumla.

Hayo ameyasema alipokuwa akizungumza katika mkutano mkuu wa ziada wa wanahisa uliofanyika tarehe 01.06.2019 jijini Dar es Salaam, ambapo ndugu; Lyaniva alisema kuwa, ili safari hiyo ya kuelekea soko la hisa iwe nzuri ni vyema wanachama wote wakashirikishwa kufanya maamuzi katika hatua hiyo ya kuelekea soko la hisa ili kuepuka manung’uniko ya wanachama kutoshirikishwa katika maamuzi hayo.

“Nimeambiwa mnakwenda kwenye soko la hisa, ninaomba nitoe maelekezo yafuatayo; Kabla hamjaenda kwenye soko la hisa ninataka na ninaelekeza wanahisa wote mridhie. Wazo limekuja , limetolewa mnaenda kwenye soko la hisa jambo ambalo ni nzuri, jambo ambalo ni la kuondoa umasikini, lakini baada ya hapo kusiwe na manung’uniko nataka wote kwa kauli moja mseme twendeni huko na mimi niwashauri nendeni kwenye soko la hisa huko ni kuzuri zaidi

alisema mkuu wa wilaya Temeke ndugu; Lyaniva.

Aidha, ndugu;Lyaniva amewataka wanachama wa kawaida wa jatu ambao bado hawajaanza kuwekeza kwa kununua hisa za Jatu kuanza kushawishika kufanya hivyo, kwani ni biashara nzuri kwa kila mtu hata kwa wale wanaoelekea kustafu.

Pamoja na hayo, mkuu huyo wa wilaya ya Temeke amewataka wanajatu kuwa kitu kimoja na kujitahidi kuhudhuria vikao vinavyoitishwa, kwani mikutano hiyo ndio sehemu pekee ya kutatua changamoto na kumaliza migongano mbalimbali katika kampuni.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Jatu Plc, ndugu; Peter Isare, akizungumza kabla ya wanahisa wa kampuni hiyo kufanya uchaguzi wa bodi mpya ya wakurugenzi ambayo pia ilichaguliwa kupitia mkutano huo, alisema kuwa, ni vyema wanabodi watakaopata nafasi hiyo ya kuchaguliwa wakatambua dhamira ya Jatu, ambayo ni kuisaidia jamii ya Watanzania katika kutokomeza umasikini kupitia kilimo, viwanda na masoko na hivyo kuwasihi kuitumikia jatu kwa uaminifu na weledi, huku wakitanguliza maslai ya wanajatu mbele na si maslai ya mtu mmoja mmoja au ya kwao binafsi.

Mbali na hayo, kupitia mkutano huo wanachama walipata nafasi ya kupata elimu kuhusu masuala ya hisa kutoka Kampuni ya Archy Financial Lt.d iliyoko chini ya ndugu, Richard Manamba, ambaye aliwaeleza wanachama wa jatu kuhusu taratibu za usajili wa kampuni katika soko la hisa pamoja na faida za kampuni kuingia katika soko hilo la hisa na manufaa anayoyapata mwanachama mmoja mmoja endapo kampuni itasajili hisa zake katika soko la hisa la DSE.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply