TAARIFA KWA UMMA

TAARIFA KWA UMMA

JATU Plc ni kampuni iliyosajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) chini ya Sheria ya Kampuni ya Mwaka 2002 na kupewa cheti cha usajii namba 130452 kilichotolewa tarehe 20 Octoba 2016. Vilevile, JATU Plc imesajiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa namba ya utambulisho wa mlipa kodi TIN 132-718-008 na imeidhinishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kama mzalishaji wa bidhaa za chakula kwa cheti Namba.2534. Aidha, JATU Plc inashirikiana na JATU SACCOS LTD ambayo ina Cheti cha Usajili Namba DSR 1655 Kilichotolewa na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika na ina leseni ya biashara Na. MSP3TCDC/2021/00143 iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania.

JATU Plc inashughulika na kilimo biashara ambapo kwa kipindi cha misimu mitano yaani ; 2017/2018 hadi 2021/2022 imefanikiwa kulima mashamba yenye ukubwa wa jumla ya ekari 40,678 kwa ajili ya kilimo cha mahindi, maharage, mpunga, parachichi, chungwa, ngano, soya na alizeti kwa kushirikiana na wanachama wake wapatao 5,000 (kati ya wanachama 38,000) ambao wanapata mkopo wa kilimo bila riba kutoka JATU SACCOS, kampuni inatumia mfumo wa kimtandao (application) uitwao JATU MARKET katika kuuza na kutoa huduma zake pia inaendesha maduka yake (supermarkets) katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mtwara na Dodoma. Vilevile, Kampuni inasambaza na kuuza bidhaa zitokanazo na kilimo kupitia mawakala wake walioko katika mikoa mbalimbali Tanzania na hutoa huduma kwa watu wa rika na jinsia zote hapa nchini.

JATU Plc iliorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) tarehe 23 Novemba 2020 baada ya kukidhi vigezo na matakwa ya kuorodheshwa katika soko la hisa (DSE Rules) na inaendelea kufuata na kukidhi matakwa ya kampuni kuendelea kuorodheshwa katika Soko la Hisa yaani Continuous Listing Obligations.

Mnamo tarehe 2 Aprili 2022 jijini Dar es Salaam, JATU Plc iliendesha kikao chake cha kawaida na Wakulima ambapo Kampuni ilitoa mrejesho kuhusu maendeleo ya mazao na malipo ya mavuno ya mwaka 2021. Katika kikao hiki, baadhi ya Wakulima walitoa malalamiko kuhusu kucheleweshwa malipo na utaratibu wa utoaji wa malipo hayo. Kutokana na malalamiko hayo Bodi ya Wakurugenzi imechukua hatua madhubuti ili kuhakikisha kwamba wakulima wanalipwa ndani ya msimu wa 2021/2022 na kila mkulima atafikishiwa ujumbe wa kuonesha muda ambao malipo yake yatafanyika.

Bodi ya Wakurugenzi inaomba radhi kwa wakulima, wanachama na umma kwa ujumla kwa usumbufu wowote uliojitokeza. Aidha, Bodi ya Wakurugenzi inapenda kuwahakikishia wakulima na umma kwa ujumla kuwa Taasisi za Serikali na wasimamizi wa Sekta husika ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) zimetoa miongozo kwa JATU Plc na kufuatilia ili kuhakikisha kwamba wakulima wanalipwa kwa mujibu wa taratibu na kanuni zilizokubalika kati ya JATU Plc na Wakulima ndani ya msimu wa 2021/2022.

Toa Jibu

Funga menu
Kiswahili
English Kiswahili