TAARIFA YA MKURUGENZI MKUU WA JATU PLC : Ndugu Peter Isare

JATU PUBLIC LIMITED COMPANY

 

TAARIFA YA MWENYEKITI

 

 

TUKIO     :     MKUTANO WA KWANZA WA WANAHISA

TAREHE :     28.04.2018

ENEO       :     UKUMBI WA TUKUYU – LANDMARK HOTEL

UBUNGO – DAR ES SALAAM

 

 

 

JENGA AFYA TOKOMEZA UMASKINI

  1. UTANGULIZI

Nitumie fursa hii kumshukuru mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uhai mimi na timu yangu yote, pamoja na wana Jatu Plc. Nimshukuru sana mama yangu mzazi kwa malezi yake mazuri kwangu siku zote, niwashukuru familia yangu mke na watoto kwa ushirikiano mkubwa na uvumilivu ambao wamekua nao kwangu kwa kipindi chote ambacho tunalijenga wazo la Jatu Plc. Niwashukuru sana waasisi wa Jatu Plc vijana wenzangu ambao siku zote tumevumiliana na kufanya kazi kwa bidi tukisubiri siku hii ya leo, niwashukuru sana wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa Jatu Plc, niwashukuru sana walezi wetu ambao ni Profesa John Palamagamba Kabudi, Profesa Bertha Omary Koda na Dokta Abdallah Gonzi kwa malezi na hekima zao siku zote tangu LPLIO had leo tupo Jatu Plc. Pia niwashukuru sana watumishi wote wa Jatu Plc katika ofisi zetu zote, mawakala pamoja na wanahisa wote wa Jatu Plc Mungu awabariki sana na atujalie umoja, ubunifu,uthubutu,bidi na tutoe huduma bora katika kampuni yetu ya kitanzania daima.

 

  1. WANAHISA WA JATU PLC

Kampuni ya JATU PLC ni kampuni ya Umma ambayo imesajiliwa kisheria na inamilikiwa na wanachama wake ambao wanajiunga kwa kiingilio na kwa uamuzi wao binafsi wananunua hisa za kampuni ili kuchangia utekelezaji wa miradi ya kampuni. Hadi sasa kampuni inawahisa 540 ambao wamenunua hisa kuanzia 50 na kuendelea na kwa ujumla wake kampuni imefanikiwa kuuza jumla ya hisa 140,879 ambazo ni sawa na asilimia 1.7% ya hisa zote za JATU PLC. Mfumo wa JATU PLC ulivyo kwa sasa unaruhusu mwanachama wa JATU anunue hisa kuanzia 50 hadi 20,000 na jumla ya asilimia 37.5% hisa zote za jatu tayari imetengwa ili iweze kuuzwa na kukamilisha mtaji wa kuendesha kampuni kwa kipindi cha miaka mitano ya kwanza kuanzia 2017.

 

Tunatambua umuhimu wa wanahisa wetu wote kwa pamoja kuanzia walioshiriki mkutano huu pamoja na wale ambao hawakuweza kushiriki katika mkutano huu, tulitamani kuona wote wanashiriki lakini yapo mambo yaliyo nje ya uwezo wetu ambayo yamelazimu tuweze kuwa na wawakilishi wachache ambao watajadili na kupitisha mikakati endelevu ya kampuni kwa faida ya wote. Tunaamini wanaJatu ni watu wenye upendo na umoja na kwa sababu hiyo chochote tutakacho jadili hapa kitapokelewa na wanahisa wote waliopo sasa na watakao kuja badae.

 

Ni vyema tufahamu kwamba sisi wanahisa ndio watu wenye maamuzi ya juu zaidi na ya mwisho katika usimamizi wa kampuni yetu ya JATU PLC. Lakini Tujue kwamba chochote tunachokifanya hapa kitabaki kuwa ni msimamo na malengo ambayo yatatumika katika kampuni yetu tu na si vinginevyo.

 

 

3. MALENGO MAKUU YA JATU

Kama kampuni, JATU PLC malengo yetu makuu ni;

  1. Kilimo
  2. Viwanda
  3. Masoko na
  4. Mikopo

 

4. MPANGO KAZI WA MWAKA 2016 – 2017

Kampuni yetu ilisajiliwa mwaka 2016, Oktoba 20 na kuanzia pale tulitengeneza mpango kazi wetu ambao ulianza rasmi mwezi Januari 2017.

 

Mpango kazi huu ulikuwa na lengo moja tu, kuhakikisha tunaonesha uhusiano katika vitendo au uhalisia ni kwa namna gani tunaweza kufanya kilimo, viwanda, masoko na mikopo ndani ya JATU. Hivyo basi bila kujali mtaji au mazingira tulilazimika kuanzisha mradi wa kilimo, kujenga viwanda, kuuza kwa mfumo wa masoko ya mtandao na hata kusajili Saccos ya JATU ili iweze kukopesha wanachama wake.

 

5. YALIYOTEKELEZWA 2017

Kwa mwaka mmoja tumefanikiwa kujenga mtandao wa masoko wa wanachama zaidi ya 5000 ambao leo wananunua bidhaa za JATU katika mikoa 11 ya Tanzania bara na visiwani. Hadi sasa tumefanikiwa kufika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Unguja Zanzibar, Tanga, Morogoro, Dodoma, Mwanza, Arusha, Kilimanjaro, na Dar es Salaam. Tumetengeneza mfumo wa kwenye simu na Kompyuta ambao unawezesha wanachama kujiunga, kuuuza, kununua, na kupata gawio la faida kila mwezi kutokana na bidhaa za JATU PLC.

 

Tumefanikiwa kujenga viwanda vidogo viwili, Kilombero tumejenga kiwanda cha kuandaa mchele katika kata ya Igima, na Kibaigwa Dodoma tumejenga kiwanda kwa ajili ya kusaga unga wa mahindi dona na sembe pamoja na kuchuja na kupaki mafuta ya alizeti.

 

Pia tumefanikiwa kuanzisha miradi ya kilimo kwa kuwasaidia wanachama wetu kupata mashamba na hatimaye kulima mazao ambayo yatatumika katika viwanda vyetu. Kwa mkoa wa Manyara wilaya ya Kiteto tumelima zaidi ya ekari 1700 za mahindi na alizeti na hadi kufikia sasa tunasubri mavuno kuanzia mwezi huu wa tano.

 

Lakini pia tumefanikiwa kusajili na kuanza kuendesha Saccos ya JATU ambayo tayari inakopesha wanaJatu kwa masharti nafuu sana pamoja na mkopo wa kilimo ambao hauna riba kabisa.

 

Lakini pia tumefanikiwa sana katika kujenga uongozi imara ambao sasa umetawanyika katika pande zote za nchi. Tumeimarisha idara zote muhimu za kampuni katika kuhakikisha kilimo, viwanda , masoko na mikopo vinafanyika kwa ufanisi.

 

6. CHANGAMOTO

Pamoja na mambo mengi makubwa na mazuri ambayo tumefanya kwa kipindi cha mwaka mmoja tu, changamoto bado zimekuwa ni nyingi sana, baadhi ya changamoto ambazo tumepitia ni pamoja na kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha kama vile majengo, mashine, usafiri na vifaa vya kiofisi. Changamoto nyingine ni uzoefu hasa katika biashara na uongozi, hivyo basi kupelekea kufanya makosa mengi sana ambayo kwa namna moja au nyingine yamekwamisha ukuaji wa kasi katika kampuni.

 

7. SULUHISHO LA HIZO CHANGAMOTO

Kwetu sisi JATU PLC kila changamoto tunayokutana nayo ni fursa na ni sehemu ya kujifunza, tunaamini pasipo na makosa hapana changamoto na bila changamoto hakuna mafanikio. Hivyo basi tumezikubali changamoto zote pamoja na makosa tuliyofanya mwaka jana lakini mwaka huu tumejipanga kutokurudia makosa, tumejifunza vyema kuhusu biashara yetu na tumejenga mfumo mzuri wa uongozi ambao bado tunaendelea kuboresha kila siku, lakini pia tumeweka vitega uchumi vingi ambavyo kwa mwaka huu vitaanza kuiingizia kampuni faida kubwa na hivyo kuweza kutatua changamoto ya vitendea kazi, lakini pia tumefikiria vyema mfumo bora zaidi wa Kukuza mtaji na kuimarisha kampuni yetu. Hapa leo tumekuja na bajeti ambayo tunaamini inatekelezeka na itatufikisha katika malengo yetu makuu ifikapo mwaka 2022.

 

 

8. MPANGO KAZI WA MWAKA 2018 – 2019

Katika mwaka huu mpango kazi wetu ni kuhakikisha misingi tuliyoweka mwaka jana tunaijenga na kuiimairisha ili iweze kufikia malengo. Tumedhamiria kwa mwaka huu tukuze mtaji wetu kupitia soko la hisa DSE ili tuweze kupanua wigo wa kiwanda cha Kibaigwa, tununue zana za kisasa za kilimo pamoja na mashine ya uchimbaji visima vya maji ili sasa tuanze kufanya kilimo cha kisasa, lakini pia tutaboresha utawala wa kampuni kwa kuajili wafanyakazi wa kutosha kila idara. Pia tutaendelea kuimarisha mfumo wa masoko wa JATU PLC kwa kutoa semina kwa wanachama na kuhakikisha usambazaji wa bidhaa unakuwa wa uhakika na haraka ili wanajatu wajenge afya na kutokomeza umaskini. Lakini pia mwaka huu tunategemea kuanza kutoa bima ya afya kwa wanaJatu kupitia Jatu Saccos Limited.

 

9. MATARAJIO YA MWAKA 2018

Tunatarajia kusajili wanachama wapya na kufikia wanachama elfu kumi na tano, mpaka mwisho wa mwaka huu. Hawa wanachama watavutiwa zaidi na sera yetu ambayo ni kuboresha kilimo, viwanda, masoko na mitaji kupitia semina na mafunzo ambayo tutakua tukiyafanya katika maeneo mbali.

 

10. MAPENDEKEZO YA BAJETI

Bajeti ya JATU PLC kwa mwaka huu ni jumla ya shilingi za kitanzania billion saba na millioni mia tano (7.5b) kama inavyoonekana katika jedwali la mchanganuo. Bajeti hii kwa ujumla wake tunapendekeza iweze kutekelezwa kutokana na pesa ambazo kampuni itauza hisa. Hata hivyo kwa mujibu wa andiko la mpango wa biashara tulionao kwa ajili ya hii billion 7.5 pesa hii itaweza kutumika kununua vifaa (asset) ambazo zitatumika kwa miaka mingine zaidi na hivyo kufanya ukuaji wa kampuni kwa miaka ijayo isijikite katika kununua mashine na hivyo kampuni sasa kwa miaka ijayo itaanza kupanua biashara yake bila kuathiri au kulazimika kuuza hisa zake nje. Hata hivyo bajeti hii ni sehemu ya utekelezaji wa bajeti ya miaka mitano ya kampuni na takwimu za upembuzi yakinifu tuliofanya kwa kutumia wataalamu unaonesha kwamba ifikapo mwaka 2022 tutakuwa na uwezo wa kutengeneza faida ya shilingi bilioni 38.7 kwa mwaka wa tano na itakuwa ikiendelea kukua zaidi kwa kila mwaka endapo kila kitu katika ulimwengu wa biashara kitakuwa sawa.

 

11. HITIMISHO

Nawashukuru sana kwa kunisikiliza na kwa michango mizuri mliyoitoa, tunaamini sasa kampuni yetu itakuwa kampuni ya kwanza Tanzania kufanya miradi mikubwa ambayo inagusa Maisha ya watanzania hasa wale wa kipato cha chini. Ninataka niwahakikishie kwamba tukio hili la leo ni njia na mwanga katika kuelekea kutimiza dira yam waka 2022. Kumbuka vision 2022 lengo lake kuu ni kuhakikisha kwamba mtanzania anakua bilionea kwa kula chakula tu.

 

Nunua bidhaa za JATU PLC upate gawio la faida, jenga mtandao wako na hakikisha kila mtu aliyeko kwenye mtandao wako anakula kilo mia moja kila mwezi na kwamba unawajulisha marafiki zako kumi wanaokula ili nao wanunue bidhaa za JATU PLC. Kwa pamoja tutatokomeza umaskini na tutabadilisha Tanzania yetu.

 

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki JATU PLC.

 

Asanteni sana,

Peter Isare

Mwenyekiti wa JATU PLC

28.04.2018

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You may use these HTML tags and attributes: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <strike> <strong>